;

Mabadiliko katika Elimu ya juu yaidhinishwa na Baraza la Mawaziri

Msimamizi wa taasisi ya kiufundi ya kibinafsi ya Machakos Institute of Technology MIT Judy Kyania akiwa afisini mwake [Standard]

Mswada kuhusu mabadiliko katika sekta ya elimu ya juu humu nchini ambao umeidhinishwa na baraza la mawaziri huku ukisubiri hatma ya wabunge umeibua hisia mseto miongoni mwa wadau katika sekta ya elimu sawa na wananchi kwa jumla

Mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa na baraza la mawaziri jumanne ya tarehe 10 mwezi februari, 2026 yalibuniwa mwaka wa 2023 ili kuruhusu kutekelezwa kikamilifu kwa mtaala mpya wa elimu wa CBE

Mageuzi hayo yanahusisha  mswada wa mwaka wa 2024 kuhusu elimu ya juu ambao unalenga kuunganisha bodi ya HELB, Hazina ya vyuo vikuu, bodi ya hazina ya taasisi za kiufundi TVET na huduma ya KUCCPS chini ya mamlaka moja ambayo itasimamia usajili wa wanafunzi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, udhamini wa elimu na mwongozo wa tasnia kwa wanafunzi

Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo msimamizi wa taasisi ya kiufundi ya kibinafsi ya Arizona International college, Alex Musangi anasema mabadiliko hayo ya taasisi za elimu ya juu ni mazuri ila anasema hayajaweka wazi masuala mengi likiwemo suala kuhusu namna wanafunzi katika taasisi za kiufundi za kibinafsi na vyuo vikuu vya kibinafsi watakavyofaidika kutoka kwa serikali 

Baadhi ya masuala anayotaka yawekwe wazi ni pamoja na suala kuhusu namna wanafunzi katika vyuo vya kibinafsi wamekua wakinyimwa mikopo kutoka kwa hazina ya HELB, suala kuhusu namna taasisi za TVET za kibinafsi na vyuo vikuu vya kibinafsi zitakavyosajili wanafunzi hasa ikizingatiwa zimekua zikitumia mbinu za kibinafsi kuwasajili wanafunzi.

Kwa upande wake msimamizi wa taasisi ya kiufundi ya kibinafsi ya Machakos Institute of Technology MIT Judy Kyania anaunga mkono mageuzi hayo akisema sasa yatafanya elimu ya taasisi za TVET kudhaminiwa kinyume na awali ambapo elimu ya TVET ilionekana kama mzigo kwa wazazi na walezi

Kyania aidha ameendelea kusifia mabadiliko hayo akisema endapo serikali itajumuisha taasisi na vyuo vya kibinafsi katika kuzitaftia wanafunzi namna inavyofanya kwa vyuo vikuu na taasisi za umma kupitia KUCCPS  itapunguza bajeti inayotumika kupitia uhamasishaji wa kusaka wanafunzi hivyo pesa hizo zitatumika kuboresha masomo 

Katika mabadiliko hayo serikali vilevile inalenga kushirikiana na taifa la Uchina ili kuweka vifaa vya kutoa mafunzo ya kisasa katika taasisi 70 za TVET ili kutoa mafunzo kwa idadi hitajika ya vijana katika juhudi za kufanikisha malengo ya ruwaza ya mwaka wa 2030

.

RELATED NEWS